img

Majogoo wawili wagombaniapo panzi hugeuka furaha ya kimburu,on August 13, 2020 at 1:42 pm

August 29, 2020

Na JAVIUS KAIJAGE KUKU wa kienyeji wanaofugwa huku wakijitafutia chakula huwa ni viumbe wa ajabu sana linapokuja suala la mawindo ya chakula chao hasa wanapokuwa katika mazingira ya kuumwa njaa kali kwa muda mrefu. Siku moja nikiwa katika kijiji fulani nilipita katika shamba la mkulima mmoja aliyekuwa na kijishamba kilichokuwa karibu na kichaka chenye majani
The post Majogoo wawili wagombaniapo panzi hugeuka furaha ya kimburu appeared first on Gazeti la Rai.,

Na JAVIUS KAIJAGE


KUKU wa kienyeji wanaofugwa huku wakijitafutia chakula huwa ni viumbe wa ajabu sana linapokuja suala la mawindo ya chakula chao hasa wanapokuwa katika mazingira ya kuumwa njaa kali kwa muda mrefu.

Siku moja nikiwa katika kijiji fulani nilipita katika shamba la mkulima mmoja aliyekuwa na kijishamba kilichokuwa karibu na kichaka chenye majani marefu.

Kimsingi mkulima huyo licha ya kuwa mkulima wa mazao mbalimbali lakini pia alikuwa mfugaji mdogo wa vijikuku vya kienyeji ambavyo wakati wa asubuhi alikuwa akiviachia vijitafutie chakula.

Kuku hao kutokana na kujitafutia chakula, wakiwa shambani humo karibia na eneo kilipokuwa kichaka ghafla alijitokeza panzi ambaye walianza kumkimbiza na mdudu huyo ili ajinusuru aliamua kukimbilia kichakani humo.

Masikini hao kuku kutokana na njaa waliyokuwa nayo waliamua kumkimbiza panzi yule hadi kichakani huku wakisahau ndani ya kichaka hicho kuwa inawezekana kunamwindaji mwingine mwenye njaa kali kuliko wao.

Mmm….kama walivyowahi kusema wahenga ya kuwa: ‘‘tamaa mbele mauti nyuma’’ ndivyo ilivyotokea kwa kuku hao waliokuwa majogoo kwani kitendo chao cha kugombania panzi waliyemkimbiza hadi kichakani iligeuka kuwa furaha ya kimburu aliyeamua kuwarukia na kuwang’ata.

Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania ni kwamba mwaka huu tutakuwa na uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa kufanyika Oktoba.

Kama ilivyo haki kisheria kwamba kila chama ambacho kimesajiriwa kina haki ya kusimamisha wagombea katika nafasi mbalimbali ndivyo ilivyo kwa sasa.

Vyama mbalimbali kuweka wagombea hasa katika nafasi ya urais hilo halina shida, lakini shida inajitokeza pale ambapo malengo ya vyama husika yanapokuwa hayaeleweki.

Tanzania ni nchi inayoendeshwa kwa mfumo wa vyama vingi ambavyo ndani mwake kuna chama tawala na vyama vya upinzani.

Malengo na mikakati ya chama tawala ni kuhakikisha kinaendelea kubaki  madarakani ilhali vyama vya upinzani malengo yao ni kuhakikisha vinakitoa chama tawala kilichoko madarakani.

La kujiuliza vyama vya upinzani hapa nchini, vinaweza vipi kukitoa chama tawala ambacho kimekuwepo tangu nchi ipate uhuru huku kikiwa kimekita mizizi yake na hivyo kuwa imara zaidi?

Swali hili linakuja kutokana na komedi ambayo nimekuwa nikiishuhudia kutoka kwa vyama vya upinzani tangu kufanyika uchaguzi mkuu wa kwanza kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1995.

Kimsingi tangu uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 vyama vya upinzani kupitia chama kimoja kimoja chenye nguvu vimekuwa  vikileta ushindani mkali, lakini kura zao zimekuwa hazijitoshelezi kwenda Ikulu na hiyo imekuwa ikitokea kutokana na kukosa umoja na ushirikiano miongoni mwao mbali na sababu nyinginezo.

Uchaguzi mkuu wa 1995 Chama cha  National Convention for Construction and Reform-Mageuzi, kupitia aliyekuwa mgombea wake Augustine Lyatonga Mrema  alikuwa  mshidi wa pili kwa kupata kura 1,808,616 sawa na asilimia 27.77 dhidi ya mgombea  wa CCM, Benjamin Mkapa aliyekuwa mshindi wa kwanza kwa kupata  kura 4,026,422 sawa na asilimia 61.82%

Vyama vingine vya upinzani vilivyosimamisha wagombea wakati huo ni: CUF – Profesa Ibrahim Lipumba kura 418,973 sawa na asilimia 6.43, UDP –John Cheyo kura 258,734 sawa na asilimia 3.97.

Uchaguzi Mkuu wa 2000 Chama cha Wananchi (CUF) chini ya mgombea wake Pofesa Ibrahim Lipumba alikuwa mshindi wa pili kwa kupata kura 1,329,077 sawa na asilimia 16.26 dhidi ya mgombea wa CCM Benjamin William Mkapa aliyekuwa mshindi wa kwanza kwa kupata  kura 5,863,201 sawa na asilimia 71.74.

Vyama vingine vya upinzani vilivyosimamisha wagombea ni NCCR –Augustine Lyatonga Mrema kura 637,115 sawa na asilimia 7.80,  UDP – John Cheyo kura 342,891 sawa na asilimia 4.20.

Uchaguzi Mkuu wa 2005 CUF chini ya mgombea wake, Profesa Ibrahim Lipumba alikuwa mshindi wa pili kwa kupata kura 1,327,125 sawa na asilimia 11.68 dhidi ya mgombea wa CCM, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete aliyekuwa mshindi wa kwanza kwa kupata kura 9,123,952 sawa na asilimia 80.28.

Vyama vingine vya upinzani vilivyosimamisha wagombea ni Chadema –Freeman Mbowe kura 668,756 sawa na asilimia 5.85, TLP –Augustine Lyatonga Mrema kura 84,901 sawa na asilimia 0.75, NCCR – Sengondo Mvungi kura 55,819 sawa na asilimia 0.49%, DP –Christopher Mtikila kura 31,083 sawa na asilimia 0.27, NLD –Emmanuel Makaidi kura 21,574 sawa na asilimia 0.19 , PPT –Anna Senkoro kura 18,783 sawa na asilimia 0.17, Demokrasia Makini – Profesa Leonard Shayo  kura 17,070 sawa na asilimia 0.15 na Sauti ya umma –Paul Henry Kyara  kura 16,414 sawa na asilimia 0.14.

Uchaguzi mkuu wa 2010 Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) chini ya mgombea wake, Dk. Wilbroad Slaa alikuwa mshindi wa pili kwa kupata kura 2,271,941 sawa na asilimia 27,05 dhidi ya mgombea wa CCM – Dk. Jakaya Mrisho Kikwete aliyekuwa mshindi wa kwanza kwa kupata kura 5,276,827 sawa na asilimia 62.83.

Vyama vingine vilivyosimamisha wagombea ni: CUF – Profesa Ibrahm Lipumba kura 695,667 sawa na asilimia 8.28, PPT –Peter Kugo Mziray kura 96,933 sawa na asilimia 1.15, TLP –Muttamwega Bhatt Mgayhwa kura 17,462 sawa na asilimia 0.21, NCCR –Hashim Rungwe kura 26,388 sawa na asilimia 0.31 na UPDP –Fahmi Nassoro Dovutwa kura 13,176 sawa na asilimia 0.16.

Uchaguzi mkuu wa 2015 Chadema chini ya mwavuli wa Ukawa mgombea wake, Edward Lowassa alikuwa mshindi wa pili kwa kupata kura 6,072,848 sawa na asilimia 39.97 dhidi ya mgombea wa CCM, Dk. John Pombe Magufuli aliyekuwa mshindi wa kwanza kwa kupata kura 8,882,935 sawa na asilimia 58.46.

Vyama vingine vilivyosimamisha wagombea ni: ACT – Anna Elisha Mghwira  kura 98,763 sawa na asilimia 0.65, ADC –Latalosa Yembe kura 66,049 sawa na asilimia 0.32, Chama cha Ukombozi wa Umma –Hashim Rungwe kura 49,256 sawa na asilimia 0.32, TLP –Machmillian Elifatio Lyimo kura 8,198 sawa na asilimia 0.05, NCCR –Jamker Malila Kasambala kura 8,028 sawa na na asilimia 0.05 na UPDP –Fahmi Nassoro Dovutwa kura 7,785 sawa na asilimia  0.05.

Katika mazingira ya namna hii unabaini kitu kimoja kwamba hakuna uchaguzi mkuu  hata mmoja ambapo vyama vya upinzani viliwahi kuungana na kumsimamisha mgombea mmoja katika kiti cha urais ili ashindane na mgombea wa chama tawala kwa maana ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika Uchaguzi Mkuu uliopita wa 2015 vyama kadhaa vya upinzani viliunda umoja wa Ukawa kupitia Chadema na kuleta ushindani mkali lakini hiyo haikutosha maana vyama vingine vilijitenga mfano ACT, ADC, TLP, NCCR na hivyo kupelekea CCM iendelee kuwa mshindi.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, hakuna dalili ya vyama vyote vya upinzani kuungana ili kuking’oa chama kilichokaa madarakani kwa muda mrefu na baya zaidi ndani ya upinzani wenyewe kuna mafahari wawili wanaogombania panzi mmoja anayeruka kuelekea kichakani.

Tundu Lissu aliyesimikwa na Chadema kuwa mgombea urais na Bernard Membe aliyesimikwa na ACT kuwa mgombea urais yote ni majogoo yanayogombania kwenda Ikulu moja kwani wote kwa pamoja wana ushawishi katika jamii kutokana na kila mmoja kuwa na historia fulani iliyomjenga awe jinsi alivyo.

Kimsingi vyama vyote vya upinzani vingekubali kumsimamisha mgombea mmoja kati ya majogoo haya mawili ambayo yanaonekana kuwa na ushawishi/mvuto mkubwa katika jamii, basi huenda CCM  ingelikuwa karibu na tundu la shimo, lakini nje ya hapo ni ndoto tupu.

Kitendo cha majogoo haya mawili kugombania ulaji kitapelekea wadhoofike na mwisho wa siku yatagawana kura, huku mnyama mkali CCM ambaye hashibi  akiendelea kuzoa kura nyingi zaidi kutokana na kuwa yeye ana mabavu yatokanayo na historia yake ya kujijenga kiafya kwa  muda mrefu.

Si tu majogoo haya mawili kutokana na kugombania mnofu kutayafanya yagawane  kura lakini pia hata saikojia ya wapiga kura ambao wangepigia kura upinzani, inaweza kubadilika na kupenda CCM kwani wapiga kura watajiuliza kwanini wampigie kura  Membe au Lissu huku wakijua hawezi kushinda kutokana na kugawanyika kwao?

Wakati Chadema na ACT-Wazalendo wakikolezwa na tamaa  ya ulafi wa madaraka hadi kuashiria kugombania Ikulu moja iliyoko kichakani Chamwino, myama mkali CCM yuko pembeni akifurahia jinsi atakavyowaangamiza walafi hawa.

Je, majogoo haya mawili yatakubali tamaa iwatawale hadi kugombania panzi mmoja anayekimbilia  kichakani au historia ya nyuma itakuwa fundisho kwao? (time will tell)

Email:  HYPERLINK “mailto:javiusikaijage@yahoo.com” javiusikaijage@yahoo.com, Simu: 0756521119

The post Majogoo wawili wagombaniapo panzi hugeuka furaha ya kimburu appeared first on Gazeti la Rai.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *