img

Kuna nini nyuma ya pazia mgao mapato Kenya?,on August 13, 2020 at 1:15 pm

August 29, 2020

NA ISIJI DOMINIC BUNGE la Seneti nchini Kenya kwa mara ya saba wiki iliyopita ilishindwa kufikia makubaliano ni namna gani mapato yatagawanywa kwa kaunti zote 47. Kumekuwa na mvutano mkali bungeni humo kufuatia mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Usambazaji wa Mapato (Commission on Revenue Allocation-CRA), ikionyesha baadhi ya kaunti kupoteza fedha huku zingine zikipata ongezeko.
The post Kuna nini nyuma ya pazia mgao mapato Kenya? appeared first on Gazeti la Rai.,

NA ISIJI DOMINIC


BUNGE la Seneti nchini Kenya kwa mara ya saba wiki iliyopita ilishindwa kufikia makubaliano ni namna gani mapato yatagawanywa kwa kaunti zote 47.

Kumekuwa na mvutano mkali bungeni humo kufuatia mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Usambazaji wa Mapato (Commission on Revenue Allocation-CRA), ikionyesha baadhi ya kaunti kupoteza fedha huku zingine zikipata ongezeko.

Kusuasua huku kwa Bunge la Seneti kupitisha njia hiyo ya mgao wa mapato kunachelewesha kaunti kukabidhiwa fedha kwa ajili ya mwaka wa bajeti 2020/21. Matumaini ya Wakenya wengi ilikuwa bunge hilo litafikia makubaliano wiki iliyopita, lakini wabunge wakapiga kura kuahirisha ili kuruhusu majadiliano zaidi.

Aliyewasilisha hoja ya kuahirisha ni Seneta wa Elgeyo Marakwet, Kipchumba Murkomen, ambaye alifanikiwa kupata kura ya maseneta 34 huku 26 wakipinga na moja akijitoa kupiga kura.

Kundi ambalo lilikuwa linaunga mkono hoja hiyo kujadiliwa na kupigiwa kura likiongozwa na Kiongozi wa Wachache Bunge la Seneti, James Orengo na Kiongozi wa Wengi bunge hilo, Samuel Poghisio, lilijumuisha zaidi wanasiasa wazee na wenye uzoefu wakati lile lililokuwa linataka zoezi hilo kuhairishwa ili kupata muda wa majadiliano zaidi na kuja na njia bora itakayokubalika na kaunti zote ilijumuisha zaidi maseneta vijana wakiongozwa na Murkomen, Johnson Sakaja (Nairobi) na Mutula Kilozno Jr (Makueni).

Maseneta waliopendekeza kujadiliwa na kupigiwa kura hoja ya CRA ya namna mapato yataweza kugawanywa ni Poghisio (Pokot Magharibi), Orengo (Siaya), Gideon Moi (Baringo), Isaac Mwaura (mbunge wa kuteuliwa), Michael Mbito (Trans Nzoia), Nderitu Kinyua (Laikipia), Fred Outa (Kisumu), Alice Milgo (mbunge wa kuteuliwa), Rose Nyamunga (mbunge wa kuteuliwa), Ochillo Ayacko (Migori), Paul Githiomi (Nyandarua), Sam Ongeri (Kisii) na Ndwiga Njeru (Embu).

Wengine ni Samson Cherargei (Nandi), Charles Kibiru (Kirinyaga), Christopher Langat (Bomet), Mercy Chebeni (mbunge wa kuteuliwa), Irungu Kang’ata (Murang’a), Naomi Shiyonga (mbunge wa kuteuliwa), Gertrude Musuruve (mbunge wa kuteuliwa), Kimani Wa Matangi (Kiambu), Susan Kihika (Nakuru), Moses Kajwang’ (Homa Bay), Margaret Kamar (Uasin Gishu), Ephraim Maina (Nyeri) na Beatrice Kwamboka (mbunge wa kuteuliwa).

Mapendekezo hayo ya CRA yanamaanisha kaunti 19 hususan kutoka maeneo yenye ukame Kaskazini Mashariki na Pwani yatapoteza Sh bilioni 17 za Kenya (takribani Sh bilioni 362) ambazo zitagawiwa kaunti zenye idadi kubwa ya watu hususan mikoa ya kati, magharibi na bonde la ufa.

Aidha inaelezwa mapendekezo hayo ya CRA yalizingatia mahitaji ya kiafya na jukumu la kifedha tofauti na ripoti ya umasikini.

Mvutano wa maseneta unadaiwa hauna uhusiano wa namna yoyote na namna CRA ilivyopanga mgao wa mapato kwa kila kaunti mbali unahusishwa na siasa. Ni siasa za ‘Building Bridges Initiative (BBI)’, siasa za ‘handshake’ na siasa za kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa Chama cha ODM, Raila Odinga, wanaunga mkono hoja ya wabunge wa seneti kujadili na kupigia kura namna mgao wa mapato kwa mwaka fedha 2020/21 utakavyogawanywa.

Awali ilionekana kama maseneta wanaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto ndiyo wangepinga na kutaka muda zaidi wa majadiliano lakini suala lenyewe limeonekana kuwagawa maseneta kiasi baadhi wamevuka makambi.

Mfano, Seneta wa Nairobi, Sakaja na mwenzake wa Makueni, Kilonzo Jr, wameungana na Seneta wa Tharaka Nithi, Kithure Kindiki, ambaye wiki chache zilizopita waliunga mkono hoja ya yeye (Kindiki) kuondolewa kwenye nafasi ya Naibu Spika.

Wengine ambao wamechukua msimamo kama wa Sakaja ni Naibu Kiongozi wa Wengi ambaye pia ni Seneta wa Isiolo, Fatuma Dullo na Kiranja wa Wengi, Farhiya Ali ambaye ni mbunge wa kuteuliwa. Wawili hawa ni watu wa karibu na Rais Uhuru na waliongoza kelele za Murkomen kuondolewa nafasi ya Kiongozi wa Wengi Bunge la Seneti.

Aidha wanasiasa wa upande wa Raila hususan Seneta wa Narok, Ledama Olekina, Philip Mpaayei (Kajiado), Prof Sam Ongeri (Kisii), George Khaniri (Vihiga) na Cleophas Malala (Kakamega) nao pia wameamua kupinga njia iliyowasilishwa na CRA japo inaonekana ingewafaidi kutokana na kuongezewa fedha.

Seneta wa Nakuru, Kihika na Seneta wa Laikipia, Kinyua, ambao wapo kambi ya Ruto wameamua kuunga mkono njia iliyopendekezwa na CRA akisisitiza Naibu Rais alikuwa jiwe lisilotakiwa ambalo sasa linaonekana muhimu.

Nakuru ni miongoni mwa kaunti ambayo itanufaika pakubwa na mapendekezo hayo na Kihika alieleza kama maoni ya kinafiki kuwa Ruto anazuia namna kaunti zitapata mgao wao kama ilivyoainishwa na CRA.

Badala yake alisisitiza ni upande wa Raila ambao unamsaliti Rais Uhuru kuhusu mjadala wa njia ya kutumika kugawa mapato hayo.

Kihika na Kinyua kabla ya kikao cha saba kujadili mapendekezo ya CRA, walikutana na wabunge wote wa makundi ya Kieleweke na Tangatanga kutoka Mkoa wa Kati na kuahidi uaminifu wao kwa masilahi ya mkoa na kuapa tu kuwa waaminifu kwa wale watakaokuwa nao katika kipindi hiki.

Wachambuzi wa siasa wanasema kuna uwezekano Chama cha Jubilee kikawachukulia hatua za kinadhamu maseneta wao Murkomen, Sakaja na Profesa Kindiki kwa msimamo wao kuhusu mapendekezo ya CRA.

Kuna uwezekano pia uchaguzi mkuu wa 2022 ndiyo chanzo cha mvutano wa mgao wa fedha za kaunti. Wapo maseneta ambao wameonyesha nia wa kuwania nafasi ya ugavana mwaka 2022 hivyo wanajaribu kushawishi fedha zaidi kwenye kaunti zao.

Mchumi maarufu nchini Kenya, David Ndii, alinukuliwa na moja ya chombo cha habari nchini humo akisema mapendekezo ya CRA yanapaswa kuachwa kwa sababu yanaenda kinyume na kanuni ya fedha za umma ambayo ni ‘usawa kwenye jamii’ kuliko kuzidisha upande moja.

The post Kuna nini nyuma ya pazia mgao mapato Kenya? appeared first on Gazeti la Rai.

,

Article Categories:
Uncategorized

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *